Narcotics Anonymous, Tanzania

Leo asubuhi, pamoja na Stefan na Hadija, tumeanzisha Narcotics Anonymous (NA) ya kwanza Tanzania hapa Maweni.

Mlevi ni mtu ambaye maisha yake yanatawaliwa na vilevi kama vile sigara, pombe na madawa ya kulevya. Ulevi ni ugonjwa ambao hatma yake ni jela, hospitali na kifo. NA ni kikundi cha watu waliotambua kuwa ulevi ni tatizo kubwa. Sisi ni walevi tunaotafuta ahueni kwa kukutana mara kwa mara. NA inadhamiria kumwezesha mtu kutokutumia tena kilevi au vilevi. Kuna sharti moja tu la uanachama - nia ya kuacha ulevi. Tunashauri uwe wazi kimawazo na ujipe fursa ya kupata ahueni.

Misingi ya NA ni rahisi na inaweza kutumiwa katika maisha yetu ya kila siku. Cha muhimu ni kwamba misingi ya NA inafanya kazi. NA haina uhusiano na kikundi chochote kingine, haina kiingilio wala ada, haina mikataba ya kusaini , haina ahadi za kutoa kwa mtu yeyote. NA haina uhusiano na kikundi au chama chochote cha siasa, dini au kutekeleza sheria, na hatupo chini ya uangalizi au upelelezi wakati wowote. Mtu yeyote anaweza kujiunga , bila kujali rangi, kabila, umri, jinsia, dini au imani. Hatujali ulitumia kiasi gani cha kilevi au vilevi, au ulivipata wapi au kutoka kwa nani, hatujali matendo yako ya zamani, hatujali kama una mali nyingi au una mali kidogo, tunachojali sisi ni nini unachotaka kufanya kuhusu tatizo lako na jinsi sisi tunavyoweza kukusaidia. Mgeni ndio mtu muhimu katika mikutano yetu yote, kwasababu njia pekee ya kuhifadhi ulichonacho ni kwa kukigawa. Tumejifunza kutokana na ujuzi wetu katika kikundi kuwa wanaohudhuria mikutano ya NA mara kwa mara ndio hufanikiwa kuachana na ulevi.

Kabla ya kuja NA hatukuweza kuyatawala maisha yetu. Tulishindwa kuishi na kuyafaidi maisha kama wenzetu. Ilibidi tuwe na kitu tofauti na tuliamini kuwa tumekipata katika vilevi. Tuliweka mbele ulevi kuliko ukoo, mke, mume, na watoto. Ilibidi tupate kilevi au vilevi kwa gharama yeyote. Tuliwaumiza watu wengi, lakini tulijiumiza zaidi wenyewe. Kutokana na kushindwa kwetu kuyakubali majukumu yetu tulikuwa tunajitengenezea matatiza. Tulionekana kushindwa kukabili maisha. Wengi wetu tulitambua kuwa ulevi wetu ulikuwa unatuua, lakini ulevi ni adui mjanja sana mwenye kuweza kutufanya tusifanye lolote kuboresha hali zetu. Wengi wetu tuliishia jela, au tulitafuta msaada kwa kupitia hospitali, dini na mabingwa wa magonjwa ya akili. Lakini njia zote hizi hazikufanikiwa. Ugonjwa wetu uliendelea kuibuka hadi tuliposaidiana kwa kupitia NA. Baada ya kuja NA tulitambua kuwa sisi ni wagonjwa, kuwa tunaumwa ugonjwa usio na tiba, lakini ni ugonjwa unaoweza kuzibitiwa na kupona inawezekana.

Tunakaribisha maoni, ushauri na maswali.