Narcotics Anonymous (NA) Tanzania
Misingi ya Narcotics Anonymous
Kama unataka tunachokigawa, na uko tayari kufanya jitihada kuipata, basi uko tayari kuchukua hatua fulani. Hii ni misingi iliyotuwezesha sisi kuushinda ulevi wetu.
1.Tulikubali kuwa hatuna nguvu zaidi ya ulevi wetu, kuwa maisha yetu yalikuwa yameshindikana.
2.Tuliamini kuwa ni nguvu yenye uwezo zaidi yetu ambayo ingeturudisha kutoka kwenye ulevi.
3.Tuliamua kusalimisha maisha yetu kwa Mungu kama tunavyomuelewa.
4.Tulijichambua kimaadili kiundani na bila woga.
5.Tulitubu kwa Mungu, kwetu wenyewe na kwa mtu mwingine hali halisi ya makosa na maovu yetu.
6.Tulikuwa tayari kumuachia Mungu atuondolee udhaifu wetu.
7.Tulimwomba Mungu kwa unyenyekevu atuondolee mapungufu yetu.
8.Tulitengeneza orodha ya watu wote tuliowakosea, na tulikuwa tayari kuwalipa fidia wote.
9.Tuliwafidia moja kwa moja watu hao, isipokuwa kama kufanya hivyo kungewadhuru wao au watu wengine.
10. Tuliendelea kujichambua kimaadili na tulipokuwa na makosa tulikubali makosa yetu papo hapo.
11.Tulitafuta kwa kupitia sala na kwa kutafakari mawasiliano na mungu kama tunavyomuelewa, tukiomba kujua nia yake na sisi na nguvu ya kuifanikisha.
12.Baada ya kupata mwamko wa kiroho kufuatia hatua hizi, tulijaribu kuufikisha ujumbe huu kwa walevi wengine, na kutekeleza misingi hii katika shughuli zetu zote.
Hii inaweza kuonekana kama kazi kubwa, na hatuwezi kuifanya yote kwa wakati mmoja. Hatukuwa walevi katika siku moja kwa hiyo kumbuka - pole pole ndio mwendo. Kuna kitu kimoja zaidi ya vitu vyote kinachoweza kutufanya tushindwe kuacha ulevi; ni kudharau au kutokujali misingi ya kiroho. Misingi mitatu ya kiroho muhimu ni ukweli, uwazi na utiifu. Tukiwa nayo hii, tutaushinda ulevi. Tunaamini kuwa mtazamo wetu ni ukweli wenyewe, kwani hakuna mfano wa tiba kama tiba ya mlevi mmoja kumsaidia mlevi mwingine. Tunaamini njia yetu ni ya busara, kwani ni mlevi mwingine tu anayeweza kumwelewa na kumsaidia mlevi mwenzake. Njia pekee ya kuachana na ulevi ni kutokurudia kutumia. Kama wewe ni kama sisi unaelewa kuwa kimoja ni kupita kiasi na maelfu hayatoshi. Tunasisitiza sana hili kwani tunajua kuwa tukitumia kilevi katika hali yoyote, au tukibadilisha kilevi, tunaufungulia upya ulevi wetu. Kuifikiria pombe kama tofauti na vilevi vingine imesababisha walevi wengi kurudi kwenye ulevi. Kabla hatukujiunga na NA , wengi wetu tuliona pombe kama ni tofauti na vilevi vingine, lakini hatuwezi kujiruhusu kujichanganya kuhusu hili. Pombe ni kilevi. Sisi ni walevi tunaobidi kuachana na vilevi vyote ili kupona.
Tunakaribisha maoni, ushauri na maswali.