Narcotics Anonymous (NA) Tanzania
NA Tanzania inatimiza mwezi mmoja tangu kuanzishwa. Ilikuwa mnamo tarehe 14 Novemba, 2006, siku ambayo Edward, Khadija na Stephane walianzisha NA Tanzania kwenye bwawa la Maweni, juu ya milima ya Usambara, kaskazini mashariki mwa Tanzania. Shukrani za dhati tunazielekeza kwa utawala na watumishi wa Maweni Farm Ltd, kwa kutengeneza mazingira yaliyowezesha tukio hilo.
Katika kuadhimisha tukio hilo la kihistoria, NA Tanzania kesho itazindua kikundi cha NA cha "Wanamapinduzi", kitakachokutana kila siku kuanzia saa kumi jioni hadi saa kumi na mbili jioni katika mgahawa wa Kawawa, mkabala na hosteli ya Kijitonyama ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mtaa wa Nzasa, Mwenge, Dar es Salaam, Tanzania.
"Wanamapinduzi" wanawaalika walevi na wasio walevi kuhudhuria mkutano huu wa kwanza na wa kihistoria wa kikundi chetu cha NA. Tunaamini na tunaahidi kuwa, ingawa mwanzo ni mgumu, pole pole ni mwendo na tiba inawezekana.
Tangu mwezi uanze, tumepokea salamu kutoka makao makuu ya NA na kutoka vikundi vya NA vilivyopo Marekani, Ulaya, Asia na Afrika. Vyote vinatutakia heri na mafanikio, na kutupongeza sana kwa kuchukua hatua ya kwanza ya kuanzisha kikundi. Wameahidi kuwa nasi hadi mwisho wa safari, na wametualika kwenye Mkutano Mkuu wa Dunia wa NA utakaofanyika Marekani mwezi wa Agosti hadi Septemba, 2007.
Hatuna mengi ya kusema leo, isipokuwa kukutakia afya njema na tunatumai tutakuwa wote kesho saa kumi jioni ili kutengeneza tena historia.
Unakaribishwa kutuma maswali, maelezo na/au ushauri kwa edward@maweni.com